Rais Jakaya M. Kikwete amemteua Ndg. Abubakar Rajab kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa - NLUPC

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi inapenda kuutaarifu umma kuwa Mh. Rais Jakaya M. Kikwete amemteua Ndg. Abubakar Rajab kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya Ardhi (NLUPC).
image
Ndg. Abubakar Rajab - Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya Ardhi (NLUPC)
Uteuzi huo wa Ndg. Rajab unaanza rasmi tarehe 19 Februari 2009 ambaye anachukua nafasi ya Profesa Afraim Hayuma aliyemaliza kipindi chake cha uenyekiti.

Ndg. Rajab alikuwa ni Katibu Mkuu Mstaafu.

Wakati huo huo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. John Z. Chiligati amefanya uteuzi wa wajumbe tisa (9) wa Tume hiyo.

Wajumbe hao ni Anunciata Peter Njombe ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji wa mifugo na Miundombinu ya Masoko kutoka Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Ndg. Edwin A. Ngonyani ambaye ni Mhandisi Mkuu wa Madini kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Mkurugenzi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Nd. Paulo S. Tarimo.

Wengine ni Ndg. Egbert N. Ndauka Mkurugenzi wa Huduma za Miundombinu wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Ndg. Angelina E. Madete ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira pamoja na Casmir S. Kyuki ambaye ni Mwandishi Mkuu wa Sheria kutoka Wizara ya Sheria na Katiba .

Wajumbe wengine ni Ndg. Albina Burra Mkurugenzi wa Idara ya Mipangomiji Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkurugenzi wa Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii Ndg. Erasmus Tarimo na Ndg. Apolinary Tamayamali kutoka Ikulu Dar es Salaam.

NLUPC ni Taasisi iliyo chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 3 ya Mwaka 1984 kwa lengo la kuratibu shughuli za uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini.

Imetolewa na:
Salome T. Sijaona - Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.